News

China yapenda kupanua ushirikiano wa pande zote na ADB: Waziri Mkuu wa China

Update Time:2025.03.26 Source: Clicks:1

 BEIJING - Waziri Mkuu wa China Li Qiang amekutana na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Asia (ADB) Masato Kanda mjini Beijing, jana Jumatatu akielezea nia ya China ya kupanua zaidi ushirikiano wa pande zote kati ya China na ADB.

Li amesema katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na msukosuko wa siasa za kijiografia na kuongezeka kwa hali ya kujihami, uchumi wa dunia umekuwa ukiimarika polepole na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na utulivu na uhakika.

Li ametoa wito kwa nchi za Asia kuimarisha mshikamano na uratibu, kufuata mfumo wa pande nyingi, kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi wa kikanda, kuvunja vikwazo vya biashara, uwekezaji na teknolojia, na kudumisha utulivu na mtiririko mzuri wa minyororo ya viwanda na usambazaji.

"Wakati huo huo, pande zote zinapaswa kuimarisha uratibu wa sera za jumla, kuzidisha mawasiliano na ushirikiano katika uvumbuzi wa sayansi na teknolojia, kuimarisha ufanisi na uthabiti wa uchumi wa Asia, kuhimili vyema hatari mbalimbali, na kushirikiana kufikia maendeleo ya pamoja," Li ameongeza.

Akibainisha kuwa ADB ni taasisi muhimu ya maendeleo ya pande nyingi katika kanda ya Asia na Pasifiki, Li amesema China inapenda kupanua zaidi ushirikiano wa pande zote na ADB, kusukuma ushirikiano katika kiwango kipya, kutimiza ushirikiano wa kunufaishana, na kutoa bidhaa zaidi za umma kwa kanda hiyo.

Waziri Mkuu huyo amesema pande zote mbili zinapaswa kuimarisha ushirikiano wa mambo ya fedha katika nyanja kama vile uhifadhi wa mazingira, maendeleo ya kijani na yenye kutoa kaboni chache, utunzaji wa wazee na huduma za afya, na kuzidisha ushirikiano wa maarifa katika nyanja kama vile maendeleo ya viwanda vinavyoibuka, mageuzi ya mfumo wa fedha na kodi, na mwitikio wa kuongezeka kwa idadi ya wazee.

"China inapenda kutumia uzoefu wake muhimu katika kupunguza umaskini na uchumi wa kidijitali na nchi zingine wanachama zinazoendelea katika Asia-Pasifiki ili kuwaunga mkono katika kukabiliana vyema na changamoto na kufikia maendeleo endelevu," amesema Li.

Kwa upande wake Kanda amesema wakati ambapo biashara ya kimataifa inazidi kuwa yenye kugawanyika, China imejitolea katika kuzidisha mageuzi na ufunguaji mlango wa ngazi ya juu, ambavyo si tu vinaleta ukuaji tulivu wa uchumi wake, bali pia vinatoa mchango muhimu katika ukuaji uchumi barani Asia na dunia kwa ujumla.

ADB inaweka umuhimu mkubwa katika ushirikiano na China, na inapenda kuchukua maadhimisho ya miaka 40 ya uhusiano ya ushirikiano wao kama fursa ya kuimarisha ushirikiano na China katika uvumbuzi wa maarifa, maendeleo ya kijani na nyanja nyinginezo, kuhimiza maendeleo ya eneo la Asia-Pasifiki, na kusukuma ushirikiano kati ya pande zote mbili kwenye ngazi ya juu.